Share news tips with us here at Hivisasa

Mtandao wa watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi almaarufu albino (The Albinism Empowerment Network), unataka mpango wa Nyumba Kumi kuhusisha watu ambao wanaishi na ulemavu huo katika jamii.

Viongozi wa mtandao huo walisema hatua hiyo ni njia moja ya kuhakikishia watu hao usalama kwa kujumuika na vitengo vya usalama katika maeneo yao.

Mtandao huo unahisi kwamba iwapo mpango huo utahusisha watu hao ni bayana kwamba wahusika watatilia maanani mikakati ya kuimarisha usalama wa zeruzeru.

Mshirikishi wa mtandao huo Anthony Korir alisema kuna haja ya kila mbinu kufanywa ili kuhakikishia watu hao usalama hasa wakati huu ambapo usalama wa zeruzeru unazidi kuyumbayumba.

“Mpango wa Nyumba Kumi ni lazima uhusishe watu ambao wanaishi na ulemavu wa ngozi, ili mpango huo utumike kutambua idadi ya watu ambao wanaishi na ulemavu huo,” alisema Korir.

Akihutubu katika warsha ambayo ilileta pamoja waakilishi wa watu ambao wanaishi na ulemavu wa Ngozi mjini Eldoret, Korir alitaka maafisa wa usalama kuwasaka na kuwatia mbaroni watu ambao walimvamia Enock Kogey ambaye alifariki katika hospitali ya kaunti ya Uasin Gishu kutokana na majereha aliyopata wakati wa uvamizi huo.

Korir aliongeza kuwa usalama wa zeruzeru unayumbayumba kutokana na madai ya kuwepo kwa watu ambao huwinda zeruzeru ili kutumia viungo vya miili yao kwa ushirikina.