Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wakazi wa kutoka Kaunti ya Mombasa wameitaja ziara ya rais Uhuru Kenyatta katika kaunti hiyo na eneo la Pwani kuwa baraka kubwa hasa katika masuala ya usalama na usafi wa mji.

Wakiongea siku ya Jumatano jijini Mombasa, wakazi hao kupitia kwa Fatma Athman ambaye ni mmoja wa wamiliki wa nyumba za kukodi katika mtaa wa Kisauni alisema kuwa tangu kuwasili kwa rais na kitengo kizima cha usalama na viongozi wa chama chake cha JAP, hakujashuhudiwa visa vya utovu wa usalama kinyume na vile imekuwa ikishuhudiwa kila mara.

Mama Fatma alisema kuwa kuja kwake pia kuchangia pakubwa mno kwa jiji hilo kuboreka na kuimarika katika upande wa usafi wa mitaa na angalau wakazi walijaribu kujiepusha na urushaji wa taka kiholela.

“Kila nikilala nyakati hizi zote Rais Uhuru amekuwa Pwani nimelala nikiwa na ukakamavu na bila kuhisi uoga wowote, kwani hapo nyuma tumekuwa tukisumbuliwa na vijana wa mtaa maarufu kama mateja ambao wamekuwa wakiwaibia wakazi, ambapo naamini ziara hii imekuwa na mchango mkubwa kwa kuboreka kwa amani na usalama kw ajumla,” alisema Fatma.

Hata hivyo, mmoja wa wakazi Simon Thoya alimpa changamoto ahakikishe kuwa anawapa vijana kazi ili waweze kutumia nafasi yao ya kukosa kazi kwa kuibia watu maskani mwao.