Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewahimiza wakaazi wa Malindi kuzingatia chama na uwezo wa mwaniaji watakaposhiriki uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi utakaoandaliwa tarehe saba mwezi Machi.
Akizungumza mjini humo siku ya Jumatatu katika kampeni za kumpigia debe mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha (Orange Democratic Movement) ODM, Joho aliwasuta viongozi wanaowataka wenyeji kuwapigia kura bila kujali vyama vyao, kwa kusema kuwa ni kupitia chama ambapo mwananchi ataweza kutathmini na kujua uwajibikaji wa kiongozi wake.
“Utajuaje huyu mtu unayempigia kura atakufanyia nini baada ya kumchagua, kupitia chama tutatakua na uwezo wa kukutetea na kutoa rasilimali huko juu na kuleta hapa mashinani,” alisema Joho.
Joho alisema kuwa wanasiasa wanaojidai kuwa wagombea huru katika uchaguzi huo ni wale walioshindwa wakati wa mchujo na sasa wanatumiwa kugawanya kura za vyama vingine.
Kwa upande wake, mwaniaji wa kiti cha hicho kwa chama cha ODM, William Mtego, aliahadi kuwa atahakikisha kuwa ardhi zote zilizonyakuliwa na wawekezaji na watu binafsi katika eneo bunge hilo zinarejeshwa kwa wakaazi.
Uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi utafanyika tarehe saba mwezi Machi ambapo ushindani unatarajiwa kuwa kati ya Baraka Mtego wa ODM na Phililp Charo wa muungano wa Jubilee.