Share news tips with us here at Hivisasa

Abiria katika kituo cha magari cha Mogonga kilichoko eneo bunge la Bomachoge Borabu kaunti ya Kisii, wamelalamikia wizi ambao unatekelezwa katika kituo hicho na watu wasiojulikana.

Jambo hilo limewalazimu abiria hao kuomba serikali kuweka maafisa wa polisi katika kituo hicho ili kukabiliana na wezi hao.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika kituo hicho cha Mogonga, wakati mwizi mmoja alipofumaniwa akimuibia abiria mmoja, abiria hao waliomba serikali kuweka maafisa wa usalama katika vituo vya magari ili wizi wa aina hiyo kukomeshwa.

Irene Bosire abiria aliyenusurika kuibiwa alisema kuwa begi aliyoibeba ilikuwa na simu pamoja na pesa alizokuwa anapelekea mtoto wake wa shule anayesoma shule ya upili ya Kenyoro.

Alisema kuwa alinisurika baada ya juhudi za mwizi huyo kugonga mwamba na kupata kichapo kutoka kwa madereva wa kituo hicho.

“Hatujui mwizi huyo alikotoka lakini alijitambulisha kama Cyrus Obeo. Alikuwa akitaka kumibia mama huyu aliyekuwa na karo ya mtoto wake lakini alishambuliwa na madereva,”alisema Cornellius Nyakebaka, dereva wa magari ya kuelekea Kisii.

“Tunahitaji serikali kuu pamoja na ile ya kaunti kutuwekea usalama kwa kuajiri maafisa wa polisi ambao watakuwa wanaweka usalama wa kituo hiki ili kukomesha wizi maana wezi wataogopa kutekeleza wizi huo,”alisema Benard Obiero, abiria.

Hii si mara ya kwanza abiria kuibiwa katika kituo hicho jambo ambalo limewapelekea kuomba serikali kuingilia kati ili kuimarisha usalama.