Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha kutetea haki za kibinadamu katika Kaunti ya Kisii kimetishia kuelekea mahakama kuwashtaki Wawakilishi katika bunge la kaunti hiyo waliofunga ofisi za serikali.

Wawakilishi hao walifunga ofisi inayosimamia fedha na ile ya karani kwa madai ya kutolipwa pesa za marupurupu ya vikao.

Wito huo umetolewa baada ya wawakilishi hao kufunga ofisi za karani na ile ya fedha za Kaunti ya Kisii siku ya Jumatano kwa kutaka kulipwa marupurupu ya vikao vinavyosemekana walisusia kuhudhuria.

Akizungumza na Waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika mji wa Kisii, mwenyekiti wa chama hicho kinachotetea haki za kibinadaumu katika kaunti hiyo, Vincent Mose alisema ni aibu kubwa kwa Wawakilishi hao kuzifunga ofisi hizo mbili huku akitishia kuelekea mahakama kuwashtaki ili wachukuliwe hatua.

“Hawa Wawakilishi wa wadi walichaguliwa kufanya maendeleo kwa wananchi bali siyo kufunga ofisi za serikali kulalamikia pesa za marupurupu ya vikao ambavyo hawakuvihudhuria hata,” alisema Mose.

Aidha, chama hicho kimeapa kuhakikisha haki za kibinadamu zinaheshimiwa kwa wananchi wote ili mwananchi wa kawaida asije akadhulumiwa tena humu nchini.