Chifu wa lokesheni ya Mochenwa, Wadi ya Gesima, Magara Makori amewaonya watu wote walio na tabia ya kuwanajizi wasichana katika lokesheni hiyo huku akiapa kuwa hatakubali vitendo vya aina hiyo.
Akiongea siku ya Jumanne katika ofisi yake wakati wa kupokea ripoti ya kila wiki kutoka kwa naibu chifu na wazee wa vijiji, Makori alisema kuwa atahakikisha kuwa viza vya aibu katika lokesheni hiyo vimekomeshwa kwa ushirikiano na wakazi walio na nia ya kuendeleza maendeleo ya kiuchumi.
Chifu huyo alisema kuwa ni aibu kubwa kupata mzee ambaye ana wajukuu akifanya kitendo cha kunajisi wasichana jambo ambalo ni la kukera katika jamii.
Aidha, alitoa tahadhari kubwa kwa watu hao na kusema kuwa hawana nafsi katika lokesheni hiyo na yeyote atakaye naswa atachukuliwa hatua ya Kisheria.
“Ni aibu kubwa kuwa na watu katika Jamii ambao nia yao ni uharibifu wa kila mara. Kwa sasa nawaonya kuwa milango yote imefungwa katika lokesheni hii na mwenye masikio asikie,” alisema Magara.
Kwingineko, aliwaomba wakazi wote kushirikiana na ofisi yake ili kuhakikisha kuwa viza hivyo vimeisha katika lokesheni hiyo na kusema kuwa ofisi yake iko wazi kwa wakazi kuripoti viza ili suluhu ya mapema kutafutwa.
Aliwaomba naibu wake na wazee wa vijiji kuwajibikia kazi yao na kusema kuwa lazima sheria izingatiwe katika shughuli za kiusalama.
Haya yanajiri baada ya mwanamume mmoja kukamatwa na maafisa wa polisi baada ya kumnajisi msichina mmoja katika eneo hilo.