Wakili Alfaxard Osoro kutoka Kaunti ya Nyamira amefadhili hospitali ya Raitigo level four vitanda, mablanketi na vitambaa ili kuimarisha sekta ya afya katika hospitali hiyo.
Hii ni baada ya hospitali hiyo iliyoko eneo bunge la Borabu, kukubwa na uhaba wa vitanda katika wadiza kujifungua, jambo ambalo lilimlazimu wakili huyo kutoa ufadhili huo.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika hospitali hiyo wakati alitoa ufadhili huo, Osoro alisema ni aibu sana wakati akina mama wanapojifungua ikiwa hawana bidhaa vinavyostahili vya kutosha.
Osoro aliomba serikali kuhakikisha kuwa hospitali zilizoko vijijini zimejengwa vizuri na kupewa dawa za kutosha na ili ziweze kutoa huduma bora za matibabu kwa watu wa sehemu hizo.
Wakili huyo alifurahishwa na ujenzi wa hospitali hiyo na kuomba huduma bora iweze kutolewa kuhakikisha wananchi wanapata matibabu kikamilifu.
“Naomba serikali iweze kujali hospitali zote kwa kuzijenga vizuri na kuhakikisha zimepewa dawa za kutosha ili wananchi kupata huduma bora,” alisema Osoro.
Wakazi wa eneo hilo walimpongeza wakili huyo kwa kutoa usaidizi huo wa vitanda na mablanketi pamoja na vitambaa na kumwomba aendelee kufanya hivyo.
“Tunampongeza wakili maana sasa akina mama wataweza kuhudumiwa vizuri hasa wanapojifungua katika hospitali hii iliyoko karibu nasi,” alisema Jane Omwanza, mkazi.