Naibu Gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amekanusha madai kuwa serikali ya kaunti inamiliki akaunti za benki 64 kulingana na baadhi ya maafisa.
Hii ni baada ya kusemekana kuwa serikali ya kaunti hiyo iko na akaunti nyingi ambazo hazijabainika ni za nini.
Akizungumza siku ya Jumanne na waandishi wa habari katika mji wa Kisii, Maangi alisema kuwa serikali iko na akaunti chache kinyume na madai hayo.
Aidha, Maangi alisema walipoingia mamlakani walipata akauti nyingi lakini wakazipunguza, huku akisema akaunti za benki ambazo wanazo kwa sasa ni chache, na ambazo ni akaunti za wizara mbalimbali na zile za maeneo bunge.
“Hapo mbeleni kulikuwa na akaunti nyingi lakini tulizipunguza, kwa hivyo naomba kuwafahamisha wananchi wa kaunti ya Kisii kuwa akaunti za benki tuko nazo katika serikali yetu ni chache na si zile 64 jinsi wengi wanasema,”alisema Maangi.
Pia naibu gavana huyo alisema serikali ya kaunti inajaribu kukusanya ushuru inavyohitajika, lakini bado hawajafikia kile kiwango walijiwekea.
Aliongezea kuwa watafanya kila wawezalo ili kuhakikisha ushuru unaokusanywa unatumika kwa namna inayostahili.