Madereva wanaotumia barabara kuu ya Kisumu-Busia wametakiwa kuwa waangalifu wakati wanapofika katika eneo la Ojola na Daraja Mbili, Maseno.
Akizungimza siku ya Jumanne, afisa wa trafiki katika eneo la Kisiani, James Kamau aliwataka madereva wa magari yote ya uchukuzi na ya kibinafsi, makubwa kwa madogo kutii sheria za trafiki wanapofika eneo hilo lenye miinuko na kona nyingi.
''Kuna haja ya kuwa na uangalifu wa hali ya juu na kutii sheria za trafiki kwa madereva wanaopitia barabara hiyo,” alisema Kamau.
Kamau alisema kwamba wachukuzi wa matatu wana tabia ya kuvunja sheria za barabara kiholela, na wanapokumbana na mkono wa sheria, ndio wakwanza kulalamika na kujitetea.
Ajali nyingi zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika eneo hilo lenye miinuko, miteremko na kona nyingi.
Aidha, waendeshaji pikipiki hasa wahudumu wa bodaboda pia walionya dhidi ya kupita magari kiholela katika eneo hilo na kutakiwa kuzingatia sheria za trafiki.