Mbunge wa Bahati ilioko katika Kaunti ya Nakuru Kimani Ngunjiri ametupilia mbali madai kuwa utawala wa mkoa umeshindwa kukabiliana na janga la pombe haramu nchini.
Ngunjiri alisema kuwa maafisa wa usalama, machifu na manaibu wao sio wa kulaumiwa kwa tatizo la pombe haramu kwani hawana mamlaka ya kuruhusu biashara ya vileo hivyo akiongeza kuwa anayewalaumu eti wamezembea kwa kazi hiyo anakosea.
Akiongea mjini Nakuru, alisisitiza kuwa si sawa kwa serikali kuu kuwafuta machifu na manaibu wao kwa madai ya kushindwa kupambana na pombe haramu kwani ni wajibu wa halmashauri ya ubora wa bidhaa nchini (KEBs) na bodi ya kukabiliana na dawa za kulevya nchini (NACADA) kufanya kazi hiyo.
Alisema kuwa hapingi wazo kwamba kuna machifu wengine wanaojihusisha na biashara ya pombe haramu lakini ni vyema kutilia mkazo kuwa wengine hawafanyi hivyo na kuwa ni vigumu kujua pombe haramu ni ipi wakati nembo halisi ya KEBs imewekwa kwa chupa ya mvinyo.
"Chifu akienda katika ukumbi wa burudani na kuonyeshwa chupa ya pombe iliyo na nembo ya KEBs iliyo halali, hawezi kukamata yeyote kwani ni dhihirisho kuwa pombe iliyomo ndani inaruhusiwa kisheria," alisema Mbunge Ngunjiri.
Aliongeza kuwa sio vyema kuwaadhibu machifu kwani waliofanya makosa ni halmashauri ya KEBs. Alilaumu maafisa wa KEBs kwa kushirikiana na wauzaji wa pombe haramu ambayo imewaua watu wengi na hivyo wanafaa kuwajibika kwa hilo.