Kamishna wa polisi katika Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa ametoa onyo kwa walanguzi wa dawa za kulevya kujisalimisha kwenye mamlaka ya idara ya polisi na kutangaza kwa hiari kuacha biashara hiyo.
Akihutubia wakazi ambao walijumuisha wazee wa mitaa pamoja na machifu na manaibu siku ya Jumatano kwenye eneo la Shikaadabu, Likoni, Marwa alisema kuwa wataanzisha operesheni ya kuenda kila nyumba kuwasaka walanguzi hao.
Marwa alidokeza kuwa serikali kuu kwa ushirikiano na ile ya kaunti kutoka maeneo Pwani imejitolea kuangamiza matumizi ya dawa za kulevya ambazo alisema zimefifisha mustakabali wa maisha ya vijana wengi kutoka eneo zima la pwani.
Kamishna huyo aliwataka viongozi ambao walihudhuria mkutano huo kukaza guu kwenye vita dhidi ya wasambazaji pamoja na watumiaji wa mihadarati.
Marwa aliwashauri vijana kutoka kaunti hiyo kujihusisha na shughuli ambayo itawanufaisha kwenye maisha yao badala ya kujiweka kwenye athari ya dawa ambazo alizitaja kuwa kikwazo kikuu kwa vijana kujikuamua kutoka lindi la umaskini.
Aliwataka wasimamizi wakuu wa vituo mbali mbali vya polisi kuweka juhudi za kupigana na jinamizi hilo la dawa za kulevya kwenye janibu ambazo zimeathirika mno.
“Ningependa kuwaona wazee wa mtaa wakishirikiana na jamii ya eneo hili pamoja na maafisa wa polisi ambao wamejukumika kupigana na matumizi na usambazaji wa mihadarati kwenye kaunti hii ya Mombasa, na kaunti nyingine kutoka hapa kanda ya Pwani kwa ujumla,” alisema Marwa.