Mwanamme mmoja mapema siku ya Ijumaa alifikishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Nakuru kwa tuhuma za wizi.
Mshukiwa huyo kwa jina Simon Ngigi alishtakiwa kwa wizi wa dumu la maji, nguo za ndani na nguo za mtoto zenye thamani ya Sh9,600 mnamo mwezi wa Julai tarehe 3 mwaka huu katika soko la Solai upande wa Rongai katika Jimbo la Nakuru.
Akijitetea mbele ya mahakama hayo, mshukiwa huyo alikiri makosa yake na kuomba msamaha huku akisema hakukusudia kutenda kosa hilo ila ni kukosa hela kulikomsababisha kuiba.
Aidha, aliiomba korti kwamba iwapo ingemhukumu impe kifungo cha nje ili wanawe wasiachwe kuhangaika, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na mahakama hiyo.
Akitoa hukumu yake, Hakimu Mkuu Doreen Molekyo alisema ni hatia kwa mtu yeyote kuiba mali ya mwezie kwa madai ya kukosa pesa na kuwa na shida huku akimshauri mshukiwa kutafuta usaidizi wakati mwingine atakapokuwa na shida wala sio kuwaibia watu.
Korti ilimpata na hatia na kumhukumu mshukiwa huyo kifungo cha miezi mitatu gerezani ama kutoa faini ya Sh15,000.