Mayatima 61 kutoka eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira wamekabidhiwa hundi ya fedha ambazo zitagharamia karo ya shule kwa muhula huu wa tatu katika shule mbalimba za eneo hilo.
Wanafunzi hao walipokezwa karo hiyo kupitia wasimamizi wao pamoja na walimu wa shule husika, sherehe ambayo iliandaliwa katika shule ya msingi ya Nyambogo eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira siku ya Alhamisi.
Shirika la mwanasiasa kutoka eneo bunge hilo kwa jina Victor Swanya Foundation liliwakabidhi wanafunzi hao ambao ni mayatima karo hiyo ili kujiendeleza kimasomo na kujisaidia nyakati sijazo.
Akizungumza kwa sherehe hiyo, mwanzilishi wa shirika hilo Victor Swanya aliwaomba wanafunzi hao kutia bidii shuleni ili waje kujisaidia nyakati zijazo.
Wakati huo huo, wasimamizi wa mayatima hao pamoja na walimu walimpongeza mwanasiasa huyo kwa kuwakumbuka na kujali maslahi ya mayatima wa eneo hilo ili kujiendeleza kimasomo.
“Tunampongeza mwanasiasa huyu kwa kile anaendelea kufanya kwa kutoa usaidizi wa karo ya shule kwa mayatima ili kuhakikisha mayatima wamesoma kikamilifu,” alisema Peter Omwanza, mmoja wa wasimamizi wa wanafunzi hao.
“Tunaomba viongozi wengine kushikana mikono na kuanza kusaidia mayatima jinsi mwanasiasa Swanya anafanya ili kila mwanafunzi yatima ama asiwe waweze kusoma na Kenya iendelee mbele,” alisema Japhet Osoro, mwalimu.
Wanafunzi nao hawakuficha furaha yao na kumshukuru mwanasiasa huy0 kwa kuendelea kuwaunga mkono kimasomo.