Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda katika eneo la Nyakoe kwenye barabara kuu ya Kisii-Oyugis Bwana Benson Nyagaka amewataka maafisa wa trafiki kuwanasa waliovunja sheria za barabara.

Nyagaka amewataka maafisa wa trafiki kutoka vituo vya Polisi vya Gesonso na Kisii Central kuhakikisha madereva na waendeshaji bodaboda wametii sheria za barabara na kuwanasa wanaopuuza sheria hizo kwa kuendesha kwa mwendo wa kasi kupita kiwango kilichowekwa cha 80 kuenda chini.

Mwenyekiti huyo aliyekuwa akizungumza na Mwandishi huyo siku ya Jumatatu alisikitikia barabara hiyo ambayo imekuwa ikitumiwa na magari mengi ambayo alisema mara nyingi huendeshwa kwa kasi mno na mengi yao yamesababisha ajali kwa wapita njia.

Aliwalaumu baadhi ya maafisa wanaopiga doria katika barabara hiyo kwa kukosa kuwachukulia hatua madereva ambao hupeleka magari kwa mwendo wa kasi na kuwataka wakuu wa vituo vya polisi kutoka sehemu hiyo kuwawajibisha maafisa hao.

Kwa upande wake Felix Chweya, mwanakamati wa wafanyibiashara ya maduka eneo hilo aliiomba serikali kuu kupitia serikali ya Kaunti ya Kisii kuwasilisha ujumbe kwa almashauri ya barabara kuu nchini KERA, kuweka matuta katika barabara hiyo ili kupunguza ajali inayoshuhudiwa kila mara katika eneo hilo.

Walisema haya siku mbili tu baada ya mtoto wa miaka 12 kugongwa na gari na kufa papo hapo wikendi jana, hiyo ikiwa ni takribani kisa cha tano mwaka huu kushuhudiwa katika sehemu ya barabara hiyo ambapo kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, vimechangiwa na uendeshaji wa magari kwa kasi na usiozingatia sharia husika za trafiki.