Polisi Nyamira wamewatia mbaroni washukiwa wawili wa wizi waliopatikana na sare za polisi na bunduki mbili za kujitengezea siku ya Jumanne katika eneo la Kebirigo.
Akithibitisha kisa hicho, OCPD wa Nyamira, Rico Ngare alisema wakazi waliwaarifu polisi kuhusu washukiwa hao jambo ambalo liliwafanya kuchukua hatua.
"Wananchi ndio waliarifu polisi kuhusu washukiwa hao hali iliyosaidia maafisa wetu kuwatia mbaroni katika eneo la Kebirigo," Ngare alisema.
Ngare aidha alisema kuwa kuna washukiwa wengine wanne ambao wametiwa mbaroni mjini Kericho huku akidinda kuwataja washukiwa hao akisema uchunguzi unaendelea ili kubaini kama visa hivyo vinahusiana.
"Polisi huko Kericho wamefanikiwa kuwatia mbaroni washukiwa wengine wanne na kwa sababu uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na visa hivi sitataja majina yao," alisema.
Kwa sasa washukiwa hao wanaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Nyamira wakingoja kufikishwa mahakamani.