Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya mkasa wa moto kuharibu nyumba ya biashara na kuteketeza mali ya zaidi millioni 50 mjini Kisii siku ya Ijumaa wiki jana, Seneta wa kaunti ya Kisii Chris Obure amewaomba maafisa wa polisi kuanzisha uchungunzi na kubaini nini kilikuwa chanzo cha moto huo.

Wito huo umetolewa baada ya kubainikia kuwa mikasa ya moto inapotokea katika kaunti ya Kisii, vyanzo vya mikasa hiyo havijawahi julishwa wananchi, na mara hii Obure ametaka kujua ni nini huwa kinasababisha mikasa hiyo kila mara.

Akizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumapili mjini Kisii, Obure aliwataka maafisa wa polisi kufanya uchunguzi haraka iwezekanavyo ili wananchi wa kaunti hiyo kujua chanzo cha moto uliochoma mali ya mamilioni ya pesa siku ya Ijumaa.

Aidha, seneta huyo aliwataka maafisa wanaosimamia mikasa na kuzima moto wakati inapotokea katika kaunti hiyo kufanya kazi yao kikamilifu, kwani waliajiriwa kufanya kazi hiyo.

“Nilishangaa sana wakati nilisikia kuwa hawa wanaosimamiia mikasa katika kaunti yetu ya Kisii hawakuwa na maji ya kutosha kuzima moto huo uliochoma mali ya watu wengi,” alisema Seneta Obure.

“Naomba wale ambao wameajiriwa kushughulikia kazi ya mikasa kufanya kazi yao kikamilifu ili kuokoa mali ya wenyewe,” aliongezea

Wakati huo huo, seneta aliwataka wazima moto katika kaunti ya Kisii kuwa na maji ya kutosha katika magari ya kuzima moto kila wakati, ili kuokoa mali ya wananchi kwa wakati ufaao.