Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Kaunti ya Kisumu, Jack Ranguma atazindua rasmi mpango wa 'Kisumu Urban Project' (KUP) katika shule mbili Kisumu Magharibi.

Ranguma ataanzia katika Shule ya Msingi ya Thim Bonde kabla ya kuelekea Shule ya msingi ya Rota siku ya Jumatano.

Akizungumza katika kikao cha maandalizi na kamati ya halimashauri ya KUP, siku ya Jumanne katika afisa yake iliyoko Manyatta, mwakilishi wa Kaunti Ndogo ya Kisumu Magharibi, Paul Obara, alisema mpango huo unanuia kuboresha elimu kwenye shule za msingi katika eneo hilo kwa kutoa ufadhili wa vifaa za elimu na kusaidia watoto kutoka katika jamii masikini.

“Elimu ya watoto wetu ni msingi wa maendeleo katika jamii ya taifa hili na ndio zawadi pekee ya mzazi kwa mwanawe. Hii ndio sababu serikali ya Kaunti ya Kisumu chini ya uongozi wa Gavana Ranguma imekua katika mstari wa mbele kukuza elimu,” alisema Obara.

Shule zilizoko maeneo ya Kajulu, Kolwa East, Kolwa Central, Manyatta B na Nyalenda A pia zimeorodheshwa kunufaika na mpango huo katika Kaunti hiyo ya Kisumu West.

Viongozi wa kidini na mashirika ya kijamii katika eneo hilo wamepokea mpango huo kwa moyo mkunjufu huku wakitoa heko kwa viongozi wa Kaunti ya Kisumu kwa kuzingatia elimu.

Kiongozi wa kanisa la Got Calvary Legion Maria, Elias Komenya alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Kisumu inajaribu sana kupambana na maadui wanne wa mwananchi, ikiwa ni, kupambana na ujinga, magonjwa, njaa na kuwapa raia wake makao.