Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali katika Kaunti ya Nyamira wameomba serikali ya kaunti hiyo kuwajengea maktaba ya vitabu ili waweze kudurusu na kusoma zaidi na kujiinua kielimu.

Wito huo umetolewa na wanafunzi wengi wa vyuo vilioko katika kaunti hiyo ambao walisema wao hupatiwa kazi nyingi ya masomo ambayo huhitaji wingi wa vitabu vya kusoma ambavyo baadhi yao haviko katika vyuo vyao.

Wakizungumza na mwandishi huyu wa habari siku ya Jumatano katika chuo cha Elgon View College tawi la Nyamira, wanafuzi hao wakiongozwa na Peter Omariba walisema kuwa maktaba ni ya muhimu sana kwa wanafunzi na kuomba serikali ya Nyamira kufikiria jambo hilo na kulitatua kwa kuwajengea maktaba hiyo.

“Wengi wetu hatuna vitabu vya kusoma. Kile ambacho tunakabidhiwa na walimu ni kidogo na tunahitaji kupata vitabu kwa wingi na kusoma lakini sasa hatuna maktaba ya vitabu hapa Nyamira,” alisema Lydia Kerubo mwanafunzi.

Aliongezea, “Ingekuwa vizuri tuwe na maktaba ambapo tunalipa hata pesa kidogo bora tusome kama vyuo vingine katika kaunti ya Kisii.”

Aidha, wanafunzi hao waliomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kuhakikisha kuwa mataa yamewekwa hadi katika vyuo vya kaunti hiyo kama njia moja ya kuimarisha usalama hasa wanafunzi wanapotembea usiku wakati wanatoka darasani kwa masomo ya ziada.

Wanafunzi hao waliungwa mkono na wanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii, tawi la Nyamira, wakiongozwa na James Onsarigo mwanafunzi wa mwaka wa nne ambaye anasomea taaluma ya ualimu.