Wafugaji na wakulima katika Kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kufurahia baada ya serikali ya kaunti hiyo kusema wakulima watakuwa wakipiga simu bila malipo kwa serikali hiyo.
Akizungumza katika uwanja wa michezo wa Gusii wakati wa maonyesho ya kilimo yaliokuwa yakiendelea siku ya Jumamosi, mkuu wa idara ya kilimo katika Kaunti ya Kisii Vincent Sagwe alikiri kuwa serikali ya kaunti hiyo imemaliza mikakati ya kuanzisha huduma ya simu ambazo wakulima watakuwa wakipiga pindi jambo mbaya linapotokea ili maafisa wa kilimo katika kaunti hiyo kulishughulikia haraka iwezekanavyo.
Wakulima mbali mbali, haswa wafugaji wa mbuzi, ng’ombe na mifugo wengine watafaidika pakubwa na mpango huo ambao kwa mujibu wa Sagwe, utanza kufanya kazi hivi karibuni.
“Tukianzisha huduma wasimu hiyo wakulima watakuwa wakipiga simu bila kulipishwa malipo yoyote na kumjulisha afisa husika shida ambayo amekabiliana nayo akiwa kwake ili kushughulikiwa,” alidokeza Sagwe mkuu wa idara ya kilimo katika Kaunti ya Kisii.
“Ikiwa ni ng’ombe amekuwa mgonjwa afisa anakimbia anamshughulikia haraka iwezekanavyo ikilinganishwa na hapo mbeleni maana mkulima alikuwa anasumbuka kumtafuta daktari na watu wamekuwa wengi katika Kaunti ya Kisii. Simu itarahisisha mambo hayo sana kwa kupasha habari idara husika,” aliongeza Sagwe.
Aidha, Sagwe alidokeza kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii imewaajiri maafisa wa kushughulikia mambo hayo kwa kila wadi zote 45 zilizoko katika kaunti hiyo.
“Tumepanga tayari jinsi maafisa hao watakuwa wakishughulikia changamoto hizo na maafisa hao watangalia jinsi ya kusaidia wakulima ili wakazi wa Kaunti ya Kisii wanufaike na huduma hiyo,” alidokeza Sagwe.