Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyibiashara wanaojihusisha na upasuaji wa mbao katika Jimbo la Nakuru wamefurahishwa na hatua ya shirika la kusimamia misitu nchini (KFS) kuwaruhusu kupasua mbao kwenye misitu ya serikali.

Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi wa shirika la KFS Emilio Mugo aliyeongea siku ya Jumatatu, wahudumu waliokaguliwa mwaka ulopita ndio watakaoruhusiwa kukata miti iliyokomaa.

Kwenye mkutano ulioandaliwa katika kituo cha kibiashara cha Turi iliyoko Wilayani Molo, wanachama wa shirikisho la wahudumu wa biashara ya mbao katika Jimbo la Nakuru walisema kuwa mfumo uliowekwa na shirika la KFS utawanufaisha wahusika wa biashara hiyo.

Mwenyekiti mpya wa shirikisho hilo Jotham Kariuki aidha alisema uamuzi huo umechelewa japo akaelezea kuridhishwa akisema ukakati wa miti imekuwa hulka ya kampuni zenye usemi mkuu.

Charles Kimata amechaguliwa kuwa katibu wa kanda ya Nakuru huku Lucy Muiruri akichaguliwa kama mwekahazina.

Shirikisho hilo lina wanachama waliojitenga na kampuni kubwa za kutengeza bidhaa za mbao na kwa sasa lina wanachama zaidi ya 1,000 kote nchini.

Akiwa ameandamana na zaidi ya wafanyibiashara 50, Kariuki alisema wanachama watahusishwa katika shughuli ya upanzi wa miti katika miezi zijazo, azma inayolenga kupanda miche milioni moja ya miti.

“Tutazidi kushurutisha ugavi sawa wa rasilimali ya miti ya serikali kati ya wafanyibiashara wadogowadogo na kampuni kubwakubwa hususan katika ukataji wa miti,” alisema Kariuki.

Wafanyibiasha hao wamekuwa wakishiriki maandamano ya mara kwa mara kushinikiza wao kupewa fursa ya kukata miti katika misitu ya serikali panapo fursa.

Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi wa shirika la KFS Emilio Mugo alisema, “Shirika la KFS linatoa kibali kukatwa kwa miti aina ya pine na cyprus kwenye misitu ya serikali. Haya ni miti iliyokomaa ilmuradi tu wanaowasilisha maombi wawe na rekodi ya kazi yao hususan katika ukuzaji wa miche ya miti.”