Share news tips with us here at Hivisasa

Wahudumu wa afya katika Kaunti ya Nyamira wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kaunti hiyo kukubali kuwapandisha wahudumu hao vyeo na kuwaongeza mshahara.

Haya yanajiri baada ya wahudumu hao katika kaunti hiyo kulalamikia mshahara duni na kutopandishwa vyeo katika kazi zao.

Serikali ya Kaunti ya Nyamira ikiongozwa na Gavana John Nyagarama pamoja na chama cha wahudumu hao cha 'Kenya Medical Practitioners Pharmacist and Dentist Union', walikubaliana siku ya Alhamisi kuwapandisha vyeo na kuwaongeza mshahara wahudumu wa afya katika kaunti hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nyamira, mwenyekiti wa wahudumu wa afya katika Kaunti ya Nyamira, Erick Aori, alisema kuwa makubaliano hayo yaliyotiwa sahihi yataafikiwa kikamilifu na serikali ya Kaunti ya Nyamira

Kulingana naye, kufikia sasa madaktari 26 kati ya madaktari 44 wamepandishwa vyeo huku wakitarajia kuwapandisha vyeo wahudumu zaidi.

Mwenyekiti wa chama cha wahudumu wa afya Samuel Oroko alisema makubaliano hayo sharti yaafikiwe kikamilifu ili uwazi kuonekana kwa wahudumu hao wa afya.

“Hii leo tumekubaliana na tumetia sahihi ili wahudumu hawa wawe wanapandishwa vyeo baada ya muda fulani na kuongezewa mshahara kama njia moja ya kuonyesha uwazi kwa wafanyikazi wa umma,”alisema Oroko.