Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wahudumu wa matatu kwenye barabara kuu ya Kisumu-Busia wameonywa dhidi ya kubeba mizigo kupita kiasi kwenye bodi ya magari yao.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika eneo la Maseno, Kamanda wa polisi wa trafiki eneo la Maseno, Wycliffe Kariuki alisema kuwa uchukuzi wa matatu unaharibiwa na madereva na utingo wao wasio na maadili mema.

Alisema kuwa msako mkali ambao uliendeshwa kwenye barabara ya Kisumu-Busia ulifichua mambo mengi ya kisiri ambayo huenda yakasababisha madhara makubwa iwapo maafisa wake hawatakuwa maakini kazini.

Alisema kuwa baadhi ya magari ya uchukuzi katika barabara hiyo hubeba abiria na mizigo kupita kiasi cha uzito unaotakikana kwa magari ya uchukuzi.

Kariuki alisema kuwa idadi kubwa ya magari ambayo husababisha ajali huwa yamebeba abiria na mizigo kupita kiasi mbali na kuendeshwa kwa kasi zaidi.

“Magari katika barabara hii hubeba mizigo mingi na abiria kupita kiasi huku yakienda mwendo wa kasi, hali ambayo imechangia ongezeko la visa vya ajali kwenye barabara hiyo,” alisema Kariuki.

Alisema kuwa utingo wa magari ya uchukuzi wameonekana maranyingi wakiwa wamekalia bodi ya gari huku gari lenyewe likiwa limebeba abiria kupita kiasi mbali na kwendeshwa kwa kasi, hali ambayo ni hatari kwa usalama wao na abiria kwa jumla.