Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wajane 520 kutoka eneo bunge la Mugirango Kusini, Kaunti ya Kisii wamefadhiliwa mablanketi kutoka shirika moja lisilo la kiserikali kwa jina Broad Kenya.

Wajane hao ambao walifadhiliwa wana miaka zaidi ya 65 na wengi wao hawana uwezo wa kujitafutia kwani wamekuwa wakongwe.

Wajane hao walipata usaidizi wa ufadhili huo katika mji wa Nyamarambe ulioko eneo mbunge la Mugirango Kusini. 

Akizungumza siku ya Jumanne katika mji wa Nyamarambe wakati ufadhili huo ulikuwa unaendelea, mkurugenzi wa shirika hilo katika Kaunti ya Kisii Josphine Bonareri alikiri kuwa shirika hilo litaendelea kuwasaidia wajane wote na mayatima katika maeneo bunge yote tisa ambayo yako katika Kaunti ya Kisii ili waweze kujiendeleza kimaisha.

“Hawa wajane ambao tumefadhili leo wengi wao wana miaka zaidi ya 65 jambo ambalo lilitufanya tuwasaidie kwani wengi wao hawana uwezo wa kujitafutia na tutaendelea kuwasaidia katika maeneo bunge yote tisa katika Kaunti ya Ksii,” alisema Bonareri. 

Aliongeza, "Wajane walio chini ya miaka 65 tunawaomba wajiandikishe kwa vikundi wapate mikopo ya kufanya biashara maana wao wako na nguvu si kama hawa ambao tumefadhili leo.”

Aidha, aliomba watu wote katika jamii kuona wajane kuwa kama watu wengine wa kawaida huku akisisitiza kuwa wajane ni watu wa maana sana kwani kupoteza waume wao si jambo walilojitakia.