Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wadi ya Sensi, Ochong’a Saisi ameahidi kuchimba visima katika wadi yake ili wakazi waweze kunufaika kwani kumekuwa na uhaba wa maji katika eneo hilo.

Tayari mradi wa maji umeanzishwa katika eneo la Nyakeiri huku sehemu zingine zikitarajiwa kufuata baadaye.

Akizungumza siku ya Jumanne afisini mwake iliyoko mjini Kisii, mwakilishi huyo alisema tayari wamemaliza mikakati ya kuweka miradi ya maji hayo ili wakazi wa eneo hilo waweze kunufaika zaidi.

“Serikali yetu ya Kaunti ya Kisii ikishirikiana nami tutaweka miradi ya maji hapa kwa wadi ili wakazi wale ambao wamekuwa wakitafuta maji kwa kutembea safari ndefu wapumzike kidogo,” alisema Ochong’a.

Aliongezea, “Miradi mingi ya maji itakuwa ikiwekwa kando kando mwa shule za serikali ili kusiwe na masuala ya fitina visima hivyo vikiwekwa katika shamba la mtu.”

Ukosefu wa maji umekuwa kero kwa watu wengi wa eneo la Sensi jambo ambalo limepata suluhu kupitia mwakilishi wa eneo hilo, ambaye alisema wakazi wa eneo hilo hawatasumbuka tena kwa kukosa maji safi.

Mwakilishi huyo aliomba wakazi kuwa watulivu na kusema atafanya maendeleo mengi zaidi katika eneo hilo kabla ya uchaguzi ujao.