Share news tips with us here at Hivisasa

Aliyekuwa waziri wa elimu na mbunge wa eneo la Nyaribari Masaba Sam Ongeri, amewataka wakazi wa eneo la Masaba kujiwekea usalama wao badala ya kulaumu serikali kila mara.

Ongeri ambaye alikuwa akizungumza katika eneo bunge hilo la Nyaribari Masaba siku ya Jumapili, alisema kuwa mbali na serikali kuwahakikishia wakazi hali ya usalama ni sharti usalama uanze nao.

Ongeri ambaye pia ni balozi kwenye Jumuia ya Umoja wa Mataifa pia aliwataka wakazi katika eneo la mpaka, kuishi kwa amani na umoja na kuepukana na mizozo ya kijamii ambayo husababisha migongano baina ya makabila ambayo hupakana.

“Nawaomba machifu pamoja na manaibu wao kuwashirikisha wakazi katika masuala ya kuleta uwiano ili kufanikisha maendeleo. Wakifanya hivyo, Kaunti za Kisii na Nyamira zitaweza kujiinua katika mambo ya kijamii, kisiasa na uchumi wa nchi kwa jumla.

Ongeri aliwashukuru wakazi kwa kudumisha umoja miongoni mwao na jamii wanayopakana nayo na kuwasihi viongozi wa siasa kutoka sehemu hiyo na kaunti za Gusii kuhubiri mshikamano wa jamii zote nchini, na kuiunga serikali mkono katika masuala ya maendeleo.

Haya yanajiri baada ya kushuhudiwa migogoro ya kikabila kwenye sehemu hiyo ambayo husababishwa na wizi wa mifugo baina ya jamii hiyo na jamii inayoishi katika mpaka wa eneo la Borabu na Bometi.