Share news tips with us here at Hivisasa

Wakongwe na watoto yatima kutoka lokesheni ya Bosongo kaunti ya Kisii wameipongeza serikali kwa kurahisisha upokeaji wa pesa za mradi wa 'Inua Jamii' kupitia benki.

Walisema hayo siku ya Ijumaa katika kambi ya chifu wa lokesheni hiyo walipofika ili kukabithiwa pesa hizo.

Walishukuru serikali huku wakisema kuwa tangu mradi huo uanzishwe wameweza kujitatulia shida kadhaa ambazo awali hawakuweza.

"Watoto yatima, kwa mfano wanaendelea kupata masomo yao kwani pesa hizi zinawasaidia kulipa karo," mmoja wao alisema.

Aidha, walipongeza mfumo huo wa serikali wa kuwapatia pesa kupitia benki la KCB na kusema kuwa umepunguza ufisadi ambao wanasema ulikuwa hapo awali.

Walisema kuwa walikuwa wanatuniwa pesa hizo kupitia kituo cha posta, njia ambayo wanasema wenzao kadhaa hawakuwa wanafikiwa na pesa zao.

"Pesa hizi zimenisaidia pakubwa. Nimewalipia wajukuu wangu wawili karo ambao ni yatima. Natoa shukrani zangu kwa serikali," Joyce Mekenye alisema.

Pia, waliwakashfu baadhi ya watu waliojiandikisha kwa njia zisizo halali wakisema wanafaidika ilhali wao sio wakongwe wala yatima.