Walimu wakuu wa shule za msingi na za upili katika Kaunti ya Kisii wameombwa kutowadhulumu wanafunzi wanaoishi na ulemavu wanapoendelea kupata mafunzo yao shuleni.
Akizungumza na waandishi wa habari afisini mwake siku ya Jumatatu, afisa wa elimu katika divisheni ya Getembe iliyoko katika wilaya ya Kisii ya Kati Ruben Migiro, aliwaomba walimu wakuu wa shule kuheshimu haki za wanaoishi na ulemavu na kuwachukulia wanafunzi hao kama wanafunzi wengine huku akisema hao ni kama binadamu wengine.
“Naomba kila mwalimu mkuu wa shule zote ambazo ziko katika Kaunti ya Kisii kutobagua na kuwaona wanafunzi wanaoishi na ulemavu kama ambao hawahitajiki na kukubalika katika jamii. Munapaswa kuwachukulia kama binadamu wengine,” alisema Migiro.
Afisa huyo pia aliwaomba wanaoishi na ulemavu kutokuwa na tabia ya kuombaomba katika mitaa tofauti na kuwaomba kujifunza cha kufanya huku akisema kuwa mtu akiwa na ulemavu sio mwisho wa maisha yake.
Migiro alisema wanaoishi na ulemavu wanaweza kujishughulisha na biashara tofauti na kuwaomba kujifunza kushona nguo ,viatu na mafunzo mengine ili kujikimu na kujiimarisha kimaisha.
“Wale wanaoombaomba wakiwa kandokando mwa barabara za mji wa Kisii naomba wajifunze kufanya biashara tofauti kama vile kushona nguo na viatu ili nao wajisaidie maishani mwao,” alisema Migiro.
Aliongeza: “Kwani wale wanaoombaomba wataomba mpaka lini ili waridhike na pesa? Huo ni uzembe ambao hauwezi saidia jamii yetu ya mkisii."