Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Muungano wa wanafunzi wa Chuo cha ufundi cha Mombasa umeahidi kufika katika bunge la kaunti ya Mombasa ili kujitetea kuhusiana na uchomaji wa magari mawili ya kaunti.

Kwenye mahojiano na mwanahabari huyu kwa njia ya simu siku ya Ijumaa, Kiongozi wa muungano huo Ocharo Ondieki alisema kuwa wako tayari kutoa ushahidi kuhusiana na waliohusika katika uchomaji huo.

Ondieki ameshikilia msimamo wake kuwa waliochoma magari hayo ni watoto wanaorandaranda mitaani wala sio wanafunzi wa chuo hicho.

Ondieki alipuzilia mbali mswada uliowasilishwa katika bunge la Kaunti ya Mombasa wa kuwataka kulipa magari hayo mawili ya kaunti hiyo yaliyochomwa wakati wa maandamano.

“Mswada huo uliwasilishwa bungeni bila uchunguzi wowote kuthibitisha kuwa wanafunzi hao ndio waliochoma magari hayo,” alisema Ondieki.

Aidha, Ondiek alisema kuwa swala hilo limeingizwa siasa ndani yake na kudai kuwa bunge la kaunti hiyo halizingatii haki za wanafunzi hao.

Vile vile kiongozi huyo amemtaka Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kubadilisha uamuzi wake wa kuwanyima ufadhili wa masomo na nafasi za kufanya mazoezi katika serikali hiyo kwani wanafunzi wengi wataumia haswa wa kutoka mkoa wa pwani.

Mwakilishi wa wadi ya Portreiz, Fadhili Mwakarani aliwasilisha mswada huo Siku ya Jumatano wiki iliyopita ya kutaka wanafunzi hao kuchukuliwa hatua za kisheria na kulipa hasara walioitekeleza.