Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanaume wawili walifikishwa katika mahakama moja ya Nakuru leo Ijumaa asubuhi kujibu shtaka la kuiba simu tatu katika eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru kwa kutumia silaha hatari.

Mahakama iliarifiwa na upande wa mashtaka kuwa mnamo mwezi Julai tarehe 3 mwaka uliopita, Dennis Kosgei na Nicholas almaarufu chitoo na wengine ambao hawakuwa mahakamani walitenda kitendo hicho huko Njoro na kuwanyang'anya Steven Ngugi na Paul Kariuki simu zao tatu za rununu.

Akitoa ushahidi wake mbele ya hakimu mkuu wa Nakuru Monica Maroro, Paul Kariuki ambaye ni mmoja wa walalamishi aliiarifu mahakama kuwa siku hiyo walikuwa wakichunga mbuzi zao ndiposa wanaume watatu walitokea wakiwa wamejihami kwa vyuma na panga na kuwaamrisha wawape simu zao.

Steven Ngugi ambaye alikuwa mlalamishi wa pili alisema mbele ya korti kuwa juhudi zao za kuwafuata washtakiwa ziliambulia patupu kwani waliwatishia maisha yao kwa silaha hatari walizokuwa nazo na hata kuonywa na mtu aliyewaona wakiwafuata kuwa washtakiwa walikuwa wezi hatari.

"Juhudi zetu za kuwakabili washukiwa hazikuzaa matunda kwani waliamuru tukae kimya na tusiende mahali popote, walitutisha kwa silaha hizo na tukafahamishwa kuwa wanaweza kutuua iwapo tungezidi kuwafuata," alisema Ngugi.

Washukiwa walikanusha kosa hilo na kudai kuwa mashahidi hawakutoa ushahidi mwafaka wa kudhibitisha madai ya wizi waliyokuwa wakiwatuhumu nayo.

Hakimu Maroro aliwaambia washtakiwa kuwa wana kesi ya kujibu na kuwaeleza kuwa kesi yao itatajwa mnamo mwezi Julai 20 mwaka huu.