Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la Kaunti ya Kisii limekubaliana kila pikipiki ipewe nambari maalumu ili kurahisha ukusanyaji wa ushuru na kuepusha ulaghai miongoni mwa wale ambao wana mtindo wa kuhepa kulipa ushuru.

Haya yalithibitishwa na kiongozi wa upinzani kwenye bunge hilo Bwana George Mokaya, kwenye hafla iliyofanyika siku ya Jumatano katika ukumbi wa Kisii Cultural, kujadili mswada wa kifedha awamu ya mwisho ambayo ilihusisha wakazi wa kaunti hiyo.

Bwana Mokaya alisema kuwa utaratibu huo uliafikiwa kama njia moja ya kupata pesa kutoka kwa waendeshaji bodaboda na kuziba njia za mkato ambazo alisema zimekuwa zikitumiwa na wahudumu hao na kumalizia kunyima serikali hela nyingi kila mwezi.

“Tulikubaliana kuwa sharti pikipiki ziwekwe nambari maalumu ili kuziba njia za waongo na wale ambao wamezoea kuepa kulipa ada kwenye kitengo chetu cha kukusanya ushuru. Mbinu hiyo itahakikisha kaunti yetu inapata hela,” alisema Mokaya.

Afisa mkuu wa masuala ya uongozi ambaye aliongoza hafla hiyo Bwana Patrick Lumumba, aliwahakikishia wakazi kuwa mswada huo hautawanyanyasa.

Alisema serikali ya kaunti inawahusisha kutoa maoni yao kwenye miswada muhimu kama hiyo ili kuhakikisha kuwa wakazi hawanyanyaswi.

Bwana Lumumba aliwashauri wafanyibiashara na wahudumu wa magari pamoja na wa bodaboda kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ifaayo wanapohisi kuwa masuala yao hayajashughulikiwa vile inavyohitajika.

Aliwaomba wakazi kushiriki kwenye mijadala ambayo huandaliwa na kaunti hiyo ili kusiwe na kutoridhika miongoni mwa wakazi.