Chifu wa lokesheni ya Omogochoro, Obed Moruri, amewaonya wakaazi dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao jambo mbaya linapotokea.
Chifu huyo alisema kuwa wakazi wanapaswa kuripoti visa kama hivyo kwa kituo chochote cha polisi ili wapate usaidizi.
Wito huo umetolewa baada ya watu kumchoma mshukiwa wa wizi msiku ya Jumapili katika kijiji cha Momoma, Kaunti ya Nyamira.
Akizungumza siku ya Jumapili katika kijiji cha Momoma, mahala mshukiwa wa wizi alipochomewa, chifu huyo aliwaonya watu kutochukua sheria mikono mwao na kusema vituo vya polisi vilijengwa kushughulikia mambo ya uhalifu.
Chifu huyo amewataka vijana ambao hawana ajira kutojihusisha na mambo ya uhalifu na kuwashauri kutafuta mbinu mbadala ya kupata chakula badala ya kuiba kwani maisha yao yatakuwa hatarini.
“Vijana wa eneo hili nawaomba kama hamna ajira mtafute kazi yoyote ya kufanya bora msikuwe mnaiba mali ya wengine. Uhalifu ni jambo mbaya na ni la aibu kwa Jamii yetu ya Gusii,” alisema Moruri.
Moruri alisema visa vya uhalifu katika eneo hilo vimeongezeka na kuwaonya wakazi dhidi ya kuvunja sheria.
Wakazi wa eneo hilo walimtaka chifu kuweka watu wa kuchunguza wale wanaotekeleza uhalifu kama njia moja ya kupunguza visa vya wizi katika eneo hilo.