Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua siku ya Alhamisi alimtunza inspekta mkuu wa polisi mjini Nakuru Penninah Kamicha kwa kitendo chake cha ujasiri ambapo alipokonya afisa mmoja wa polisi wa kiume bunduki.
Afisa huyo wa kiume alidaiwa kuwa amelewa akiwa na sare rasmi za kazi alipoanza kutishia kuwapiga risasi mafundi wa kutengeneza magari katika mji wa Nakuru katika barabara ya Oginga Odinga.
Afisa huyo aliyejulikana kama Noor alionekana kusumbua wenzake wa kiume waliotaka kumpokonya bunduki hiyo kwani alionekana kutisha kuwafyatulia.
Hali hiyo ambayo ilidumu kwa muda wa saa moja ilisababisha inspekta Kamicha kutumia mbinu za hali ya juu ili kumpokonya silaha hiyo na akafanikiwa. Afisa huyo alikamatwa na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nakuru.
Jambo hilo lilimfanya Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kumzawadi Kamicha fursa ya kuwa mgeni wake wa heshima katika ofisi yake iliyo mjini Nakuru. Mbugua alimpongeza sana kwa tendo hilo la kishujaa ambalo lilizuia maafa ambayo Noor angelisababisha iwapo hangenyang'anywa bunduki hilo.
Gavana Mbugua alisema inspekta Kamicha alikuwa ameonyesha ukakamavu na ujasiri wa hali ya juu katika kikosi cha polisi na amefanyika kielelezo chema sio tu kwa idara ya usalama bali kwa jamii kwa ujumla.
"Inspekta Kamicha ametenda jambo la kijasiri na ameonyesha ukakamavu mkubwa kwani iwapo hangefanikiwa kumpokonya bunduki afisa yule, tukio lake lingalikuwa ya hasara mno," alsema Gavana Mbugua.