Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae ameombwa kujenga vyoo katika soko la Kenyenya liliyoko eneo bunge la Bomachoge Borabu.
Wito huo umetolewa na wafanyibiashara wa soko hilo pamoja na wakazi wa eneo hilo ambao walisema hawana mahala pa kujisaidia wanapoendelea na shughuli zao za biashara katika soko hilo.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika eneo hilo la kenyenya, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Paul Mainga walisema wamekuwa wakishuhudia watu wengi wakijisaidia katika kichaka kilichoko karibu na soko hilo kufuatia ukosefu wa vyoo, jambo ambalo limeharibu mazingira ya eneo hilo.
Waliomba Gavana Ongwae kuwajali na kuwajengea vyoo katika soko hilo kama njia mojawapo ya kutunza mazingira.
Aidha, wafanyibiashara hao walisema kuna uwepo wa kuagiza mifugo wote ambao hufugwa katika soko hilo kuondolewa kwani viwango vya biashara vimeinuka sana katika soko hilo.
Mifugo aina ya mbuzi wamekuwa wakifugwa katika soko hilo jambo ambalo wanataka lishughulikiwe.
“Tunaomba serikali ya kaunti kupitia gavana Ongwae kutujengea vyoo katika soko letu na kuwahamisha mbuzi wanaofugwa sokoni ili tuendelee na maisha ya biashara kikamilifu,” alisema Joel Orina mfanyibiashara.