Naibu kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu Christopher Wanjau ameonya watumishi wa umma ambao wana mazoea ya kukodisha nyumba za serikali kwa watu ambao siu wafanyikazi wa umma.
Wanjau alisema kuna ongezeko la watumishi wa umma ambao wanatumia nyumba za wafanyikazi wa umma kujipatia mapato ya ziada kwa kujifanya wamiliki wa nyumba hizo.
Akihutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumanne mjini Eldoret, Wanjau alisema kuna wafanyikazi wa serikali ambao hupewa nyumba za serikali na baadaye kukodisha nyumba hizo kwa watu ambao sio wafanyikazi wa umma kwa ada ya juu zaidi.
Wanjau alisema tabia hiyo ni hatia kwa mujibu wa sheria ya nyumba na makazi kwa watumishi wa umma.
“Tumeanzisha msako dhidi ya watu wenye tabia hii baada ya kupokea ripoti nyingi kuhusu tabia hii. Wale ambao watapatikana wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ambazo husimamia nyumba husika,” alisema Wanjau.
Haya yanajiri baada ya askofu mmoja mjini humo kudai kudhulumiwa baada ya kufurushwa kutoka katika mojawapo wa nyumba za umma baada ya kuachiwa nyumba hiyo na mfanyikazi wa umma ambaye alihamia Mombasa.
Askofu Bilioni Ebole wa kanisa la Oasis of Destiny International alipinga kuhamishwa kwake huku akidai kuwa alikuwa katika nyumba hiyo kihalali baada ya kutoa malipo ya ziada ya nia njema ya Sh30,000 kwa mmiliki wa awali wa nyumba hiyo.
Tangu alipe ada hiyo askofu Ebole alisema amekuwa akilipa kodi ya Sh6,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miaka mitatu tangu ahamie katika nyumba hiyo.