Mwenyekiti wa maonyesho ya kilimo na ufugaji wa mifugo katika kaunti ya Kisii Julius Bosire amesema maandalizi yamekamilika katika uga wa michezo wa Gusii.
Aliwaomba watu kujitayarisha kujionea mengi yanayohusu kilimo pamoja na ufugaji wa mifugo mbalimbali kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 12 mwezi ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika mji wa kisii, mwenyekiti huyo alisema maandalizi yamekamilika na maonyesho hayo yatakuwa na usalama wa kutosha hadi yakamilike ili kusikuwe na vurugu yoyote.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo alisema watu wazima watakuwa wakilipishwa shillingi 200 huku watoto wakilipishwa shiilingi 150 ili kupata tiketi ya kuingia katika maonyesho hayo.
“Vikundi vilivyojiandikisha kuja katika maonyesho ya kilimo hapa Kisii mwaka huu ni vingi sana. Vikundi hivyo vilikuwa 113 lakini kufikia sasa ni vikundi 31 ambavyo vimehitimu kupata fursa hiyo na tayari vimefika katika mji wa Kisii wakisubiri maonyesho hayo kufunguliwa rasmi,”alisema Julius Bosire.
“Mwaka uliopita tulikuwa na vikundi 20 vilivyokuwa katika maonyesho haya ya kilimo lakini mwaka huu ni vikundi vingi na tunatarajia vingine kwa hivyo naomba watu waje kwa wingi kushuhudia maonyesho hayo,” aliongeza Bosire.
Maonyesho hayo hufanyika kila mwaka ili kuwafunza wakaazi jinsi ya kufuga mifugo wakiwa nyumbani mwao na hata jinsi kilimo hufanywa na kuleta mazao mengi kwa kukabiliana na janga la jaa katika sehemu mbalimbali.
Naibu kamishena wa kaunti ya Kisii alitangaza kuwa watu wote watahakikishiwa usalama wa kutosha wakati wa maonyesho hayo na kusema watu wasiogope lolote maana usalama umeimarishwa.