Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amewarai wanasiasa na wananchi wote wa kaunti hiyo kuwapa viongozi walio mamlakani nafasi ya kuleta maendeleo.

Akizungumza siku ya Jumanne katika uwanja wa shule ya msingi ya Kebere wakati chifu wa lokesheni ya Kebere Geoffrey Abuga alikuwa ankabidhiwa mamlaka ya kuwa chifu mpya wa eneo,  Maangi aliomba wanasiasa na wananchi kuwapa viongozi muda kutimiza ahadi kabla ya kuanza kuwakosoa na kuingiza siasa zisizo za kujenga taifa.

“Wale wanaotaka uongozi nawaomba muwe na subira maana wakati huu ni wa maendeleo wala si wa siasa. Nawaomba mukome kutukosoa kabla hatujamaliza kutekeleza yale yote ambayo tumeorodhesha kama viongozi kufanyia wananchi wetu,” alisema Maangi.

Maangi pia aliwaomba viongozi wote kuheshimiana, kushirikiana na kushikana mikono kufanya maendeleo kwa wananchi wa kaunti hiyo.

Wakazi nao walifurahishwa na matamshi ya naibu gavana huyo kuhusu umoja miongoni mwa viongozi wote wa kaunti huku wakisema yale wananchi wanahitaji ni maendeleo.

“Na sisi kama wananchi tunahitaji umoja kutoka kwa viongozi wetu maana haya mengine ya kuvutana hapa na pale hayawezi kutusaidia kamwe. Tunataka viongozi watufanyie maendeleo,” alisema Lilian Obiri, mkazi.