Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amewashtumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa madai ya kueneza porojo ya kuharibu uhusiano wake na Gavana Ongwae.
Aliwataka adui zake kufanya maendeleo kwa wakazi wa kaunti hiyo badala ya kujihusisha na siasa za 'kubomoana' ambapo alisisitiza uwepo wa mshikamano na umoja wa kufanya kazi pamoja na viongozi wengine ili kuimarisha uchumi wa Kaunti ya Kisii.
Naibu huyo wa gavana alikuwa akizungumza Jumatano jioni katika ukumbi wa michezo na utamaduni mjini Kisii wakati wa kuwapokeza watu walio na ulemavu wa ngozi al maarufu zeruzeru ambapo alionyesha kutofurahia kwake kwa kuhusishwa na visa vya baadhi ya wakazi walioandamana hivi majuzi kwenye mtaa wa Ogembo, hali ambayo alisema inaweza kusababisha ukosefu wa imani kwa wananchi na viongozi wao.
Kwingineki Maangi alisema yeye na Gavana Ongwae wataendelea kufanya kazi pamoja kuinua maisha ya wakazi wa kaunti hiyo. Pia aliwahakikishia wanaoishi na ulemavu kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii itaendelea kuwapigania kwa hali na mali ili kufikia malengo yao.
"Tukumbuke wale wasio na uwezo, wale wanaoishi na ulemavu ili wajikimu maishani, na tupo na mpango wa kuinua maisha ya wakazi wote hapa Kaunti ya Kisii na tuache kuhubiri chuki," alisema Maangi, Naibu Gavana wa Kisii.
Maidai ya uhusiano baina ya naibu huyo na Gavana Ongwae yaliibuka hivi majuzi baada ya baadhi ya wakazi wa Ogembo kudaiwa kuandamana wakipinga uongozi wa Gavana Ongwae.