Huku onyo ikitolewa dhidi ya waganga kwenye kaunti ya Mombasa, mwenyekiti wa madaktari wa mitishamba, amewataka madaktari wakutoa huduma hizo kutoka kaunti sita za pwani kujiandikisha rasmi na jumuia ya waganga ya kitaifa.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Mombasa, mwenyekiti huyo Mohammed Kidzao, alisema kuwa sharti waganga wote wajisajili na muungano wa shirikisho la kitaifa la waganga hao ili kuweza kutambuliwa na kuinua imani baina yao na wateja wao badala ya kufanya kazi yao katika njia za kutiliwa shaka.
“Ni vema kila tabibu, kujiunga na jumuia ya kitaifa ya madaktari wa dawa za kiasili, na kuhakikisha kuwa dawa wanazotumia zimefanyiwa uhakiki wa kitaalamu ili ziweze kupewe wateja wao. Ni vizuri watu wajue kuwa miti ya asili hutibu asilimia kubwa ya maradhi,” alisema Kidzao.
Alidokeza kuwa hivi karibuni wanapanga kuanzisha utathmini na uhakiki wa kila mhudumu anayetumia dawa za asili, na kuwahimiza wahusika kuwa tayari kujiwasilisha kwenye msako huo.
Hatua hii imetangazwa siku mbili tu baada ya kamishna wa Kaunti Mombasa Nelson Marwa kutangaza vita dhidi ya waganga ambao wameweka mabango mitaani.
Tayari askari wa kaunti pamoja na wale serikali kuu wameonekana wakiyang’oa mabango hayo.