Mahakama moja mjini Naivasha ilifanya kikao spesheli katika Kituo cha polisi cha Gilgil siku ya Jumanne ambako kulipatikana takriban lita 5,000 za Chang’aa.
Waliokuwa wakiisafirisha pombe hiyo walifanyiwa kesi katika kituo hicho.
Mahakama hiyo ya Naivasha ilihamishia huduma zake kwa muda katika kituo hicho cha polisi, kwani ilikuwa vigumu kwa polisi kusafirisha pombe hiyo hadi mjini Naivasha.
Licha ya oparesheni kali iliyofanywa na maafisa wa polisi, wanasiasa na wananchi kwa jumla, kumaliza pombe haramu humu nchini, sasa imebainika kwamba wafanyibiashara wa pombe haramu wamebuni mbinu mpya ya kusafirisha chang’aa kutoka nchini Uganda hadi nchini Kenya bila ya kujulikana.
Pombe hiyo ilipatikana baada ya lori lililokuwa likiisafirisha magunia 52 kuhusika katika ajali eneo la Gilgil.
Magunia 21 yalikuwa yamebeba maharagwe, huku mengine yote yakiwa yamewekwa makaratasi ya plastiki ndani yake, yaliyokuwa yamejazwa pombe hiyo haramu.
Watu watatu waliokamatwa walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Naivasha Esther Kimilu na kukiri mashtaka yao.
Akitoa hukumu yake, Hakimu Kimilu alisema kwamba mahakama ilitilia maanani kwamba washtakiwa walikuwa wamepatikana na hatia kwa mara ya kwanza, na kwa hivyo, akawaagiza kulipa faini ya Sh300,000 kila mmoja, ama watumikie kifungo cha mwaka mmoja gerezani.