Mbunge wa Mugirango Kusini, Manson Nyamwenya, ameiomba serikali kuu iwalipe walimu nyongeza yao ya mshahara jinsi mahakama ilivyoagiza.
Wito huo umetolewa baada ya walimu kutishia kugoma iwapo hawatalipwa nyongeza yao ya kati ya asilimia 50 hadi 60 kulingana na uamuzi wa mahakama jambo ambalo lilimpelekea mbunge Nyamweya kuomba serikali kuwapa pesa zao kabla ya wao kugoma na masomo kutatizika.
Akizungumza siku ya juamapili katika hafla ya kuchangisha fedha ya ujenzi wa kanisa ya kikatholiki ya Nyamagwa iliyoko kaunti ya Kisii, mbunge huyo aliomba serikali kuwapa walimu pesa zao ili waendelee kuwafundisha wanafunzi.
“Walimu wanastahili kupata haki yao kwa kuongezewa mshahara wao. Naomba serikali iwalipe ili walimu wasigome kwani watoto wetu ndio wanasumbuka,” alisema Nyamweya.
Matamshi ya mbunge huyo yaliungwa mkono na mbunge wa eneo bunge la Bobasi Steve Manoti, mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo, mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kisii Mary Otara pamoja na mwenyekiti wa bodi ya KICC James Omingo Magara ambao walihudhuria hafla hiyo na kusema walimu wanastahili kupewa mishahara yao.
Aidha, mbunge Steve Manoti aliomba walimu kutogoma na kuwahakikishia kuwa serikali inaendelea kutafuta mbinu ya kuwalipa na kuwaomba waende shule kuwafunza watoto.
“Naomba walimu msigome kwani huu ndio mwanzo wa muhula na wanafunzi wanastahili kuanza kupokezwa masomo mara moja maana wameka nyumbani kwa siku nyingi sana. Wanastahili kufunzwa na tunawaomba mume na subira kidogo kwani mshahara mtapata,” alisema Manoti.
Zaidi ya Sh3.7m zilichangishwa katika hafla hiyo huku Rais Kenyatta akituma mchango wake wa Sh500,000.