Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Kitutu Chache ya Kati Richard Onyonka amewataka viongozi kutoka upinzani kuacha kuingiza siasa kwa kila mradi unaoendelezwa na Serikali Kuu kwa maeneo hayawakilishwi na wabunge wa chama cha Jubilee.

Akiongea siku ya Jumanne na Waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa zoezi la usajili wa vijana wa Huduma kwa taifa almaarufu NYS katika eneo bunge lake, Onyonka alihapa kuwa atashirikiana na Serikali kwa miradi ambayo itawafaidi wanainchi kutoka eneo bunge lake ili kuwafaa kina mama pamoja na vijana ambao ndio wengi katika taifa la Kenya.

Pia Mbunge Onyonka alisikitikia mtindo ambao umevuma miongoni mwa wanasiasa kutoka upande wa upinzani wa kulalamika mara kwa mara bila kutoa suluhu kwa Serikali na kuwasihi wenzake kukumbatia mazuri kutoka upande wa Serikali ya Jubilee na kupuuza yasiowafaa huku akisema kuwa hiyo itakuwa njia mojawapo ya kuwafaidi wakaazi wote bila kuzingatia mrengo wa kisiasa wanaunga mkono.

“Tuwe watu wa kushukuru na kupongeza kile tunaona ni kizuri kutoka upande wa Serikali badala ya kuwa watu wa kutoa lawama na kuweka dosari mahali ambapo haipo,” alisihi Mbunge Onyonka.

Mbunge huyo wa chama cha CORD amekuwa akifanya kazi na Serikali ya Jubilee kwa siku za hivi karibuni hasa masuala ya kimaendeleo ambapo hata hivyo kwa kipimo sawa amekuwa akiwakilisha chama chake cha upinzani kwa njia sawia.

Zoezi hilo lilishuhudia zaidi ya vijana zaidi 1,300 wakisajiliwa ambapo watasaidia kufanya usafi katika mji wa Kisii vile vile kujenga na kuyakarabati makao duni viungani mwa mji huo.