Wizara ya nyumba na ujenzi katika Kaunti Ndogo ya Maseno imewataka wananchi kupanda miti mbali na nyumba za kuishi.
Kauli hiyo imetolewa na katibu mtendaji katika afisi hiyo, Boston Okila aliyetuma ujumbe huo kupitia kwa watawala kwenye mkutano wa naibu wa chifu ulioandaliwa katika eneo la Chulaimbo.
Kwenye mkutano huo ulioandaliwa siku ya Alhamisi, Okila aliwaambia wananchi kwamba kuna haja ya kufanya mpangilio wa upanzi wa miti kwenye maeneo ya makazi.
''Kumekuweko na ripoti za matukio mbalimbali ya majanga ambayo yametokea baada ya miti iliyo karibu na makazi kuangukia nyumba,'' alisema Okila.
Akihutubu kwenye mkutano huo, naibu wa chifu kata ndogo ya Masianyi, George Anyanga aliwaambia wananchi kushirikiana na maafisa wa utawala kila wakati wanapotekeleza mambo mbalimbali ya kimaeneleo katika jamii.
Alisema kuwa hali ya kupanda miti hadi karibu na nyumba imechangiwa na upungufu wa ardhi, ambapo kila mtu amesalia na sehemu ndogo ya kipande cha shamba ambayo anataka kufanya kila kitu pale.
''Tushirikiane pamoja ili kufanikisha kila hatua katika maisha mbali na kuimarisha jamii zetu kimazingira,'' alisema Anyanga.
Miti iliyopandwa karibu na mijengo imekuwa ikianguka na kusababisha madhara makubwa yakiwemo maafa ya watu.