Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa muungano wa kitaifa wa wazazi tawi la Nyamira ameiomba serikali kuwalipa walimu mishahara yao.

Akiongea na wanahabari kwenye mkahawa mmoja huko Nyamira siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa muungano wa wazazi tawi la Nyamira, Bw Vincent Ombura, alisema kwamba serikali inawadhalilisha wazazi kwa maana hata wazazi huumia zaidi kwa kulipa karo bila walimu kuwepo madarasani.

"Serikali ya Jubilee inaendelea kuwadhalilisha wazazi wa taifa hili kwa maana sisi ndio tunaondelea kuumia zaidi kwa maana karo tunazolipa bila walimu kuwepo darasani ni hasara kubwa kwa wazazi,” alisema Ombura.

Mwenyekiti huyo wa chama cha wazazi ametishia kuishtaki serikali mahakamani iwapo haitawalipa walimu nyongeza yao ya mishahara kwa wiki mbili zijazo, huku akimsihi Rais Uhuru Kenyatta kutatua mzozo uliopo mara moja.

“Chama cha wazazi kipo tayari kuishtaki serikali kuu mahakamani iwapo haita walipa walimu nyongeza waliyopokezwa na mahakama ya rufaa kwa wiki mbili zijazo. Namsihi Rais Uhuru kutatua mzozo huu kwa haraka," alisema Ombura.

Akizungumzia swala la kuheshimu sheria, mtetezi huyo wa maslahi ya wazazi alisema kwamba serikali ya Jubilee imo mamlakani kwa kuidhinishwa na mahakama ya rufaa nchini baada ya mzozo wa uhalali wa kuchaguliwa kwake kuibuliwa na chama cha Cord kilichopeleka kesi mahakamani kupinga uchaguzi huo.

Alishangazwa ni kwa nini serikali hiyo haitaki kuheshimu uamuzi wa mahakama.

“Inafahamika bayana kuwa serikali ya Jubilee imo mamlakani kutokana na kuhalalishwa kwa kuchaguliwa kwake na mahakama hiyo hiyo iliyowapa nyongeza walimu, na tunashangazwa na ni kwa nini serikali sasa haitaki kuheshimu uamuzi wa mahakama hiyo?" aliuliza Ombura.

Bwana Ombura aliwaomba walimu kutotishika kwa lolote na kuendelea na mgomo wao hadi pale serikali itakapo heshimu uamuzi wa koti wakuwapokeza nyongeza yao ya mishahara.

"Nawaomba walimu kutotetereka kwa lolote wanapoendelea kupigania haki zao kwa maana ni mahakama iliyoamua wapewe haki hiyo,” alisema Ombura.