Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanamke mmoja kutoka mji wa Nakuru aliyedaiwa kumjeruhi mwanamume mmoja ameachiliwa huru na mahakama ya Nakuru.

Korti hiyo iliarifiwa kuwa mnamo mwezi Juni tarehe 28 mwaka huu, mshukiwa Lydia Chepng’eno alitenda tendo hilo kwa kumpiga kwa chupa ya pombe mlalamishi aliyefahamika kama Benjamin Mukhwana katika baa ya Nessut, madai ambayo Chepng'eno aliyakiri mbele ya hakimu mkuu wa Nakuru Doreen Mulekyo.

Mshukiwa aliangua kilio mahakamani na kuomba korti imuachilie huru kwani alikuwa na watoto waliokuwa wakimtegemea kama kitega uchumi.

Aliarifu korti kuwa mlalamishi alimshika kwa nguvu nywele zake alipokuwa kwenye baa hiyo akifanya biashara, jambo lililomfanya kuchukua hatua hiyo.

Kiongozi wa mashtaka alisema kuwa mtuhumiwa alimjeruhi mlalamishi bila sababu yoyote usoni kwa kutumia chupa ya pombe na aliumia na kufanyiwa usaidizi wa kwanza katika hospitali ya Wilaya ya Njoro na ndipo ikaripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Njoro na mshtakiwa akakamatwa.

Hakimu Doreen katika uamuzi wake alisema kuwa madai ya upande wa mashtaka yalikuwa hayana ukweli wowote kwani haingewezekana mtu wa akili timamu kushambulia mwenzake bila sababu yoyote na kama walikuwa na ushahidi wowote kuwa mlalamishi hakumtendea mshukiwa tendo lolote kesi hiyo ingechukua mkondo mwingine.

"Kiongozi wa mashtaka inapaswa kutafuta undani wa swala hili na kutoa ushahidi kamili na haiwezekani mtu mwenye akili timamu kujeruhi mwenzake bila sababu," alikariri Hakimu Doreen.

Hakimu huyo alisema kuwa amemuachilia mtuhumiwa huru kwani upande wa mashtaka haukutoa ushahidi mahususi ili kumhukumu mshtakiwa.

Hata hivyo Hakimu Doreen alimsihi mshtakiwa kuwa anapotendewa tendo lolote lisilo halali anapaswa kuarifu Askari ili sheria ichukue mkondo wake na kuwa asichukue sheria mkononi mwake.