Mwanamume mmoja alasiri siku ya Jumatano alizua sokomoko katika eneo la Soko Mjinga, Kwa Rhonda mjini Nakuru, baada ya kupanda kwenye mlingoti wa nguvu za umeme na kutisha kujiua kwa sababu ya kusumbuliwa na mkewe.
Jamaa huyo ambaye tumelibana jina lake kwa sababu sasa hivi ni mshukiwa anayetarajiwa kufikishwa mahakamani, alinusurika kupata kichapo kutoka kwa wananchi waliokuwa na hasira kufuatia kitendo chake cha kuwa na nia ya kujitoa uhai.
Polisi wakiongozwa na mkuu wa Kituo cha Polisi cha Bondeni Pascal Kiamba, walilazimika kumwokoa na baadaye kamtia nguvuni jamaa huyo.
Mwanamume huyo alipanda kwenye mlingoti huo wa umeme akitishia kujiua huku akidai mkewe hampi amani nyumbani mwake.
“Sioni faida ya kuishi. Heri nife niondoke duniani kuliko kuendelea kuvumilia usumbufu wa mke wangu,” alisema jamaa huyo huku umati uliokusanyika ukimsihi ashuke.
Aidha, jamaa huyo hakufafanua mkewe hampi amani kivipi. Mwanzoni alikaidi wito wa wananchi na hata ule wa afisa Kiamba wa kushuka na kuacha kujaribu kujitoa uhai.
“Msikaribie hapa, la sivyo nazigusa nyaya hizi za umeme,” aliuonya umati wa watu uliojaribu kumsihi ashuke.
Majirani yake walisema jamaa huyo ambaye amejaliwa kupata watoto wawili lakini hafiki nyumbani kila jioni kwani amekuwa mlevi chakari ingawaye alikuwa amenza kubadili tabia siku chache zilizopita.
“Lakini hivi majuzi, mshukiwa anafika nyumbani mapema na hii imewafurahisha watoto wake na mkewe. Lakini jamaa hawezi kukimu mahitaji ya familia yake na anasema mama amezidi na ndipo alipenda kufika nyumbani akiwa mlevi chakari,” alisema jirani yake Paul Masinde.
Mkuu huyo wa Polisi aliwaomba wananchi kuvumilia na kumpa nafasi kusema na mshukiwa na ndipo akakubali kushuka.
Afisa Kiamba alisema jamaa huyo atahojiwa na hatimaye kushtakiwa na kosa la kuhatarisha maisha yake akiongeza kuwa wananchi wa sehemu hiyo wana tabia ya kupanda milingoti wa nguvu za umeme wakijaribu kujitoa uhai.