Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume mmoja ambaye ni baba wa watoto wawili anaendelea kuuguza majeraha mabaya ya kuunguzwa kwa maji ya moto na mkewe baada ya mzozo wa kijamii.

Bw John Muchina ambaye baada ya kupokea huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Molo alihamishwa hadi Hospitali ya St. Mary’s iliyoko eneo la Gilgil kwa matibabu zaidi, alisema malumbano kati yake na mkewe yalizuka pindi tu alipofika nyumbani kutoka kazini.

Muchina alisema mkewe alimfahamisha kwamba walikuwa wametofautiana na mama mkwe alipokuwa akifanya kazi ya kuvuna mharagwe katika shamba lao lililoko eneo la Mukinyai ndiposa ugomvi ulitokea na kupelekea mkewe kurejea nyumbani majira ya mchana kabla ya kukamilisha kazi aliyokuwa akifanya.

Aidha Muchina alidokeza kuwa licha ya kuwepo kwa mizozo ya mara kwa mara kati yao hajawahi dhania mkewe angeweza kumvamia na kumchoma kwa maji ya moto akiwa usingizini.

“Tunapokuwa na mzozo wa aina yoyote, sisi hutatua na kisha kupatana. Sijui ni kwa nini leo akaamua kunifanyia unyama sampuli hii,” alisema mwathiriwa Muchina.

Alisema wakiwa na mkewe bi Beatrice Wambui, wamejaliwa watoto wawili mmoja wa kiume na mwingine wa kike huku akisema ameshtushwa na msururu wa matukio haswa baada ya kugundua kuwa mkewe alikuwa amenunua petroli pamoja na kuhifadhi upanga uliotiwa makali nyumbani kwao hivi majuzi tayari kufanya balaa.

Bw Njenga Matendo ambaye ni mshauri wa maswala ya kijamii amekilaani kitendo hicho huku akiwataka watu walioko katika ndoa kutafuta ushauri kutoka kwa wazazi, wazee wa vijiji ama viongozi wa kidini kabla ya kutumia hasira ambazo hupelekea hasara na kuvunjika kwa ndoa.

Matendo amesema changamoto za kijamii zimeongezeka kwa viwango vikubwa haswa miongoni mwa vijana akisema kitendo hicho cha unyama ni ukiukaji mkubwa wa haki na maadili ya kijamii.

“Kile nakipendekeza kwa familia ni kutatua mizozo kwa mbinu taratibu. Sio vyema kudhuru mwenzako kwa sababu ambazo iwapo masikilizano yangepewa nafasi, suluhu lingepatikana," alisema mshauri Matengo.

Kisa hicho kimelaaniwa na wakazi wa tabaka mbali mbali wakisema kuna njia nyingi za kutatua mizozo zinazozuka katika familia bali sio kwa vitendo vya kinyama na kinyume na sheria.

Matukio ya wanaume kudhulumiwa na wake zao yameongezeka nchini huku baadhi ya waathiriwa mara nyingi hukatwa hata sehemu zao za nyeti pamoja na kuchomwa kwa maji ya moto.

Mwanamke huyo ambaye aliingia mafichoni baada ya kitendo hicho anaendelea kusakwa na maafisa wa polisi.