Waziri wa usalama wa ndani Bwana Joseph Nkaisserry amewataka viongozi wote kutoa kanda ya Pwani kushirikiana ili kuweza kuangamiza makundi ya uhalifu ambayo alisema yamejikita katika kaunti za kanda hilo.
Akiongea siku ya Ijumaa wakati wa kuzindua rasmi operesheni ya kuwafurusha wahuni na magaidi wa al-Shabaab kutoka msitu wa Boni huko Lamu, waziri huyo alisema kuwa ushirikiano baina ya viongozi kutoka kaunti zote sita kutoka pwani na serikali ya kitaifa utafanikisha vita dhidi ya magaidi ambao mara nyingi wamelenga nchi ya Kenya.
Aliwapa changamoto maafisa wakuu wa polisi wa vikosi maalumu vya kupambana na ugadi pamoja na jeshi la KDF kushikana mikono kutoa ujumbe na habari za kuwanasa magadi ambao alisema walitorokea kwenye baadhi ya misitu ya eneo zima la Lamu, ambalo liko karibu sana na mpaka wa nchi ya Somali.
Aliwaonya vijana pamoja na viongozi wa kidini wenye siasa kali za kuwafundisha vijana kutoka eneo la pwani kuingia kwenye kila alichoita jihad, kwa kusema kuwa juhudi zao hazitafanikiwa kamwe kwani mkono wa serikali u macho.
Aliwataka wale wana nia kama hiyo kuachana nayo kabisa kabla sheria kuwaandama.
“Ningependa kuwaomba wazazi kuwa makini wanapoona watoto wao wakiwa na mienendo ambayo ni ya kutilia shaka na kuripoti kwenye mamlaka ya polisi au kwenye viongozi wa mtaa ili kuepusha vijana kupotoshwa na magaidi,” alisema Nkaisserry.
Nkaiserry aliwataka wakazi walio karibu na msitu huo wa Boni kuhama kutoka eneo hilo ili kujiepusha na mashambulizi ya vifaa vya kivita wakati wa makabiliano baina ya wanajeshi wa KDF na maharamia hao wa al-Shaabab.