Mwenyekiti wa kamati ya kusimamia miradi ya bunge la kaunti ya Nyamira, Peter Maroro, amemkosoa gavana wa kaunti ya Nyamira, John Nyagarama, kwa kuwarudisha kazini maafisa sita waliosimamishwa kazi kufuatia madai ya utumizi mbaya na uvunjaji wa pesa za serikali ya kaunti hiyo.
Kulingana na Maroro, Gavana Nyagarama angesubiri na kuunda kamati mpya kuwachunguza maafisa hao sita kabla ya kuwarejesha kazini.
Akizungumza siku ya Jumatano mjini Nyamira, Maroro alipinga vikali jambo hilo la kuwarudisha kazini maafisa hao sita huku akisema sharti uwazi uonekane kwa wakazi wa kaunti ya Nyamira.
Kamati mbili hapo awali ziliundwa kuwachunguza maafisa hao waliohusishwa na madai ya ufisadi lakini baadaye zikawasilisha ripoti tofauti ambazo hazikuambatana, jambo ambalo lilimfanya spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko, na wawakilishi wengine kukataa na kuzifutilia mbali ripoti hizo..
Kamati ya 'Select committee' iliyoundwa iliwasilisha ripoti yake ya kuwaondolea maafisa wanne kati ya sita madai ya ufisadi huku kamati ya 'Implementation committee' ikiwasilisha ripoti ya kuwaondolea madai ya ufisadi maafisa wote sita jambo ambalo liliwafanya wawakilishi wa wadi kuzifutilia mbali ripoti hizo zote kwa kutokuwa na uhakika.
Gavana Nyagarama aliwarudisha maafisa hao kwenye idara mbalimbali kando na zile walizokuwa wakiziwakilisha kabla ya kusimamishwa kazi.
“Baada ya ripoti zilizowasilishwa bungeni kufutiliwa mbali kwa kutokuwa na uhakika kwa uchunguzi uliofanywa, Gavana Nyagarama angeunda kamati mpya ili kuwachunguza na sio kuwarudisha kazini,”alisema Maroro.
Maafisa ambao walirudishwa kazini Miongoni mwao ni Kepha Osoro, aliyekuwa katika Idara ya Barabara, na sasa atawakilisha Idara ya Mazingira na Maji, John Omanwa aliyekuwa katika Idara ya Pesa na sasa atawakilisha Idara ya Biashara na Utalii katika Kaunti ya Nyamira.
Andrew Ombati aliyekuwa katika Idara ya Mazingira sasa atakuwa katika Idara ya Usimamizi kwa Wananchi, huku Peter Omwanza akisalia katika Idara ya hapo awali ambayo ni ya Vijana na Michezo katika Kaunti hiyo ya Nyamira.
Maafisa wengine wakuu waliorudishwa kazi ni Fridah Nyaboga Idara ya Elimu, na Ernest Morara Idara ya masuala ya michezo katika Kaunti ya Nyamira.
Maroro alipinga hatua hiyo na kusema hakuna uwazi ulioonekana.