Polisi wameanza msako mkali dhidi ya washukiwa wawili wanaodaiwa kuwateka nyara watoto wanne walikokuwa wakicheza katika uwanja wa michezo, Kikuyu.
Akizungumza siku ya Jumamosi, mkuu wa polisi katika eneo la Kikuyu, Mutune Maweu alisema kwamba wazazi wa watoto hao waliripoti kupotea kwa watoto wao waliokuwa katika uwanja wa kandanda wakicheza.
Alisema kwamba mmoja wa wale waliokuja kuripoti ni mwanadada mmoja aliyeshuhudia na kuona wanaume wawili, mmoja katika gari aina ya probox na mwingine akiwaingiza ndani ya gari.
Maweu alisema wawili hao waliendesha gari kwa kasi walipoona wanaonekana. Hata hivyo, alisema kuwa polisi wameanza msako mkali dhidi ya wawili hao ili kuweza kuwanasua watoto walioko kati ya miaka saba na kumi.
Alisema kwamba visa vya utekaji nyara vimeongezeka kwa kipindi cha miezi sita hivi, na watekaji nyara hao walikuwa wakidai pesa kiasi fulani ili kuweza kuwachilia watoto.
Hata hivyo, Maweu aliwaonya wazazi dhidi ya kuzungumza na kufuata kile ambacho wateka nyara hao wanachoamrisha.
"Wazazi wengi huaribu uchunguzi wetu wanapoanza kufuata wanachoamrishwa na hata kutoa pesa. Nawaonya wazazi dhidi ya hiyo, bali watuache tutekeleze kazi hiyo,” alisema Maweu.
Maweu aliwatahadharisha wazazi dhidi ya kuwaacha watoto wao pekee yao na kuwasihi waripoti watu wanaoshukiwa hasusan wale wanao onekana wakiwa katika eneo ambalo watoto wanacheza kwa kuwa nia yao yaweza kuwa mbovu.
Alisema pia ni juhudi ya mzazi kuhakikisha kuwa amemfunza mtoto wake asiwe anazungumza na watu asiyowajua.