Mbunge wa Kisauni ameshtumu vikali hatua ya maafisa wa polisi kuwahangaisha wakazi wa eneo la Kisauni walipokuwa wakimsaka mshukiwa wa ugaidi.
Akiongea katika eneo bunge la Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Rashid Bedzimba alisema kwamba hatua ya maafisa hao wa polisi kuwahangaisha wakazi na wengine kujeruhiwa kwa tuhumu za kumsaka mshukiwa wa ugaidi ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Bedzimba alisema kwamba hatua kama hiyo inafaa kusitishwa mara moja kwani nyumba za wakazi ziliharibiwa pamoja na milango na madirisha kubomolewa wakidai kumsaka mshukiwa wa ugaidi.
“Sisi kama wakazi wa Kisauni tumechoshwa na hatua ya maafisa wa polisi jinsi wanavyotuhangaisha kila mara wanapotuvamia wakidai wanawatafuta wahalifu. Ikiwa kuna wahalifu basi mbona wasije kumshika ili sisi tuishi kwa amani,” alisema Bedzimba.
Aidha, ameikata idara ya usalama nchini kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuvamia nyumba za wakazi ambao wanaishi kwa amani na kuchangia hofu ya ukosefu wa usalama miongoni mwa wakazi.
Kiongozi huyo amewashinikiza wakazi iwapo wanahabari kuhusu mshukiwa yeyote wa ugaidi ama mhalifu kuchukua hatua kuripoti kwa maafisa wa polisi ili kuzuia kuhangaisha na maafisa wa polisi.
Tayari wakazi wanne wameandikisha taarifa kwa maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Nyali kwa kujeruhiwa na maafisa hao ili hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya maafisa wanaokiuka haki za kibinadamu.